Social Icons

Tuesday, March 27, 2012

Hatuli tena vyakula, bali tunakula vinavyofanana tu na vyakula!


Vyakula vingi tunavyokula watu wengi duniani hivi sasa ni mfano tu wa vyakula halisi tunavyopaswa kuvila kama ilivyo historia ya binadamu tangu enzi za mababu zetu. Staili ya maisha yetu imebadilika, aina nyingi ya vyakula tunavyokula ni vile vyenye mafuta na sukari nyingi na kula au kutokula kabisa vyakula vyenye virutubisho muhimu kwa miili yetu.

Kutokana na ulaji huo wa vyakula usio sahihi, miili yetu imejikuta imejaa mafuta mabaya na sumu za kila aina kutoka kwenye vyakula tunavyokula, ama kwa kujua au kwa kutokujua na matokeo yake mfumo mzima wa kibaiolojia mwilini haufanyikazi tena, hivyo mwili kuwa rahisi kushambuliwa na magonjwa mbalimbali hatari.

Asilimia kubwa ya watu wengi duniani hivi sasa wanakula aina ya vyakula vinavyotengenezeka kwa urahisi (Fast Food) na vile vilivyokwisha tayarishwa na kuhifadhiwa kwa matumizi ya muda mrefu (Processed Foods) na biashara ya vyakula hivi imekuwa kubwa sana duniani inayoingiza mabilioni ya fedha kila siku.

Utayarishaji na upatikanaji wa vyakula hivi ni rahisi sana, lakini unagharimu afya na uhai wa maisha yetu. Utumiaji wa vyakula hivi kwa wingi na kuacha vile vya asili, ndiyo umetufikisha hapa leo ambapo magonjwa hatari kama vile kisukari, presha, magonjwa ya moyo na saratani, yamekuwa ni magonjwa yanayoua watu wengi kila siku.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Wizara ya Afya kupitia Hospitali ya Ocean Road ya jijini Dar es Salaam, ambayo inajishughulisha na kutibu wagonjwa wa saratani, jumla ya watu 100 (mia moja) hufariki dunia kila siku nchini Tanzania kutokana na magonjwa mbalimbali ya saratani. Hii ni idadi kubwa na inatisha, lakini magonjwa yote haya yanaweza kuepukwa iwapo watu watarejea kula vyakula asilia.

Maisha ya wengi wetu yako hatarini kwa sababu zaidi ya asilimia 90 ya vyakula tunavyokula kila siku iendayo kwa Mungu ni vile vya kutengeneza (Processed Food), kuanzia unga tunaoutumia kupikia ugali, mafuta tunayopikia, sukari tunayoitumia, mikate tunayokula na hata maji tunayokunywa, vyote hivi vimepitia kiwandani kwanza ambako vimeondolewa uasili wake.

Tatizo hilo lipo pia kwenye vinywaji baridi ambavyo vinawekwa kiasi kingi cha sukari huku vikiwa havina aina yoyote ya virutubisho bora au chakula asilia ndani yake. Makampuni mengi ya kutengeneza vinywaji baridi yanalaumiwa kwa kutumia sukari bandia (artificial sweeteners) ambayo inaelezwa kuwa na kionjo kijulikanacho kwa jina la ‘aspartame’ ambacho kinadaiwa kuwa na madhara kwenye ubongo wa binadamu.

Kilichopo ni uelewa na kuchukua hatua. Hatuna budi kukumbuka kwamba vyakula asilia ndiyo asili ya binadamu, kula vyakula vingine, bila kujali vinasifiwa kiasi gani kwenye matangazo ya biashara, havina msaada wowote wa kiafya katika miili yetu.

Ni kweli kwamba wakati mwingine umaskini wetu unatufanya tusiwe na uwezo wa kuchagua kilicho bora, lakini hata unapokuwa na huo uwezo unajua kwamba wewe unayekunywa uji wa dona usiokuwa na sukari na kipande cha kiazi, unakula chakula bora kuliko yule anayekunywa chai ya maziwa na mayai ya kukaanga?

Makala haya ni sehemu tu ya makala nyingi ambazo tumeshayaandika na tutaendelea kuandika kuhusu ulaji sahaihi utakaokusaidia kuwa na mwili wenye afya bora na wenye uwezo wa kukukinga na maradhi sugu, unachotakiwa kufanya ni kuuwezesha mwili kwa kula vyakula sahihi. Kumbuka kwamba, ukiutendea wema mwili, nao utakutendea wema kwa kukulinda na maradhi!







No comments:

Post a Comment

Thank you for your comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...