Social Icons

Friday, May 11, 2012

Moyo Ungekuwa Wa Kioo, Wengi Tusingekuwa Pamoja


NINA imani wote mu wazima kwa uwezo wa Mungu, hali yangu nazidi kumshukuru Muumba kwa kuendelea kunipa upendeleo wa kuendelea kuvuta hewa yake ya bure. Nazidi kukushukuru msomaji kutokana na kuniunga mkono katika kila mada ninayoandika.

Mada ya wiki jana imeonyesha jinsi gani simu zilivyogeuka sumu ya ndoa zetu, kuna mtu alituma ujumbe na kusema, tunakumbuka shuka wakati kumekucha, eti tayari ndoa nyingi zimeshavunjika kwa ajili ya simu.
Namini hatujachelewa, kwani hakuna kipya chini ya jua zaidi ya kukumbushana ili tusiyafanye makosa waliyoyafanya wenzetu, pengine hawakupata nafasi ya kusoma mada hizi kama wewe.
Basi nawe usivunje ndoa yako kwa jambo linaloweza kuepukika na mwisho wa siku useme ungejua. Nina imani nimesomeka vizuri, sasa tuendelee na mada yetu mpya kama inavyosomeka hapo juu.
Nataka nikupe changamoto moja, jiulize hivi “Wanaokaa pamoja wote wanapendana? Jibu lipo wazi, si wote wanaokaa pamoja wanapendana.
Swali lingine: “Kwa nini wapo pamoja mpaka leo hii na wengine wanapata wajukuu na hata kufa pamoja? Najua kabisa kwa akili ya juujuu unaweza ukakataa kwamba kuna watu hawapendani halafu wanaishi pamoja.
Twende pamoja ili kila mmoja aamini kile nitakachokizungumza na fanya uchunguzi kisha utanipa jibu.
Katika uhusiano wowote, si wote wanaopendana kwa mapenzi ya dhati, wapo wanaompenda mtu kutokana na tamaa za mwili au kitu.
Mara nyingi mwenye mapenzi ya dhati huwa mmoja aliyeanza au aliyepokea, kuna mmoja lazima atakupenda kwa dhati na kuamini wewe ndiye tiba yake.
Lakini upande wa pili huwa kwa ajili ya kitu fulani ambacho kina maslahi kwake na si mapenzi ya dhati kutoka moyoni.
Kama moyo ungekuwa na kioo na kuyaona anayowaza mwenzako, nina imani mapenzi yangeongezeka au kuvunjika kabisa. Kama ukijua uliyenaye anawaza makubwa juu yako lazima mapenzi yataongezeka, lakini kama ukigundua uliyenaye yupo kwa ajili ya kitu fulani na si mapenzi ya dhati, huwezi kupoteza muda wako kuendelea kuwa naye.
Tumeshuhudia watu wakijiua kwa ajili ya mapenzi kwa vile mpenzi wake hakusoma mawazo ya mapenzi ya dhati yaliyokuwemo moyoni kwa mwenzake.
Pia tumeshuhudia mtu akivunja penzi bila sababu kwa vile tu hakuwa na mapenzi ya dhati kwa mwenzake.
Aliyekuacha ghafla ungeyasoma mawazo yake usingeteseka kwa vile ungejua uliyenaye upo naye kwa ajili ya kujirusha tu na wala si mapenzi ya kufa na kuzikana.
Unajiuliza hivi; unakaa vipi na mtu asiyekupenda hata kufika hatua ya kuzeeka pamoja? Jibu ni jepesi, wengi huamini ipo siku watampata mtu aliye sahihi lakini kwa bahati mbaya huwakosa na kuishia kuvumilia mpaka mwisho.
Hujaona mwanamke au mwanaume aliye ndani ya ndoa anachanganywa na mtu wa pembeni? Sababu ni hiyohiyo aliyenaye hakumpenda bali aliishi naye kimazoea na kujikuta siku zinakatika akiwa naye, matokeo yake ndoa au mapenzi ya aina hiyo huwa ya mateso.
Nina imani nimeeleweka vizuri, ila napenda kuwaeleza wote wenye tabia hizo, heshimu muda wa mwenzio. Heshimu upendo wake, kwani yeye anajitolea kwa asilimia mia kwa vile hajui yaliyo moyoni mwako. Siku zote mpende akupendaye, utakuja penda pasipo penzi, halafu utasema hukuambiwa.
 
Shukrani kwa GPL.
Kwa story zaidi kuhusu mahusiano ingia HAPA
 



1 comment:

Thank you for your comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...