Social Icons

Tuesday, September 11, 2012

IMANI YA KWAMBA UNAWEZA NI SILAHA YA MAFANIKIO YAKOMAISHA siku zote yanaendeshwa kwa kufuata taratibu na kanuni ambazo mwisho wake humfanya mwanadamu kuishi kwa amani na furaha na kuweza kutimiza lengo lake la kuwepo hapa ulimwenguni.
Ifahamike kwamba, kila mtu ana wajibu wake ambao anatakiwa kuutimiza kwa kipindi chote ambacho atakuwa hapa duniani lakini kukamilisha wajibu huo kunawezekana kwa mtu jasiri mwenye imani kwamba hakuna linaloshindikana kwake.
Kuamini huko ni miongoni mwa sababu inayoweza kumfanya akatenda mambo makubwa aonekane ni muhimu katika watu ndani ya jamii anayoishi. 
Ndiyo maana kila ninapozungumzia suala la mafanikio huwa nasisitiza sana kila mtu kuwa na imani kwamba anaweza kufanikiwa kama walivyofanikiwa waliotangulia na kama itatokea akashindwa, nayo itakuwa ni hatua ya kuelekea kwenye mafanikio.
Imani inaweza kumfanya yeyote akatenda mambo makubwa sana na ndiyo maana wataalam wa saikolojia wanaeleza kwamba, unapotaka kufanya kitu chochote kwanza jenga imani kwamba unaweza! Hiyo itakupa nguvu na kukuwezesha kutimiza lengo ulilokusudia.
Wapo watu waliokuwa masikini sana kiasi kwamba katika fikra za harakaharaka huwezi kudhani kwamba maisha yao yanaweza kubadilika na wakaishi maisha ya kifahari. 
Lakini kwa kuwa waliamini kuwa ipo siku, sasa hivi ni miongoni mwa watu wanaotembea vifua mbele kwa mafanikio makubwa waliyoyapata. 
Hii imekuja baada ya kuukubali umasikini wao na kuuchukulia kama pointi ya kuanzia kuelekea kwenye utajiri.
Siku zote hawakuridhika bali walipambana huku wakiamini kuwa watatoka katika dimbwi la umaskini. Wewe pia unatakiwa kuishi katika mazingira hayo huku ukitanguliza imani katika kila jambo unalolifanya. 
Amini unaweza kwani hiyo ni moja ya silaha wanayoitumia watu wengi waliofanikiwa. Waliamini kwamba wanaweza, wakajaribu na hata walipodondoka walisimama na kuendelea kupambana mpaka wakatimiza ndoto zao. 
Vivyo hivyo kwako, kama wewe ni mfanyabiashara amini unaweza kuwa maarufu na kwa jitihada zako utafika huko. 
Kama wewe ni mwanafunzi, amini unaweza kufika chuo kikuu na kuwa miongoni mwa wasomi wakubwa nchini kama tu utaweka jitihada zako katika masomo.
Nalazimika kusema haya kutokana na ukweli kwamba, kuna watu ambao wenye uwezo mkubwa sana wa kufanya mambo lakini wameendelea kuishi chini ya kiwango kutokana na udhaifu wa imani zao kwamba wao hawawezi. 

Imani yako ya kwamba unaweza inaweza kukufikisha mbali kwa kutimiza ndoto zako kama ilivyotokea kwa wengine.
 Wengi walio katika hali duni kimaisha siyo kwamba Mungu amependa wawe hivyo bali wameamua wenyewe kuyasusia mafanikio wakiamini kwamba wao hawawezi kuendesha magari ya kifahari kama ilivyo kwa wengine.
 Wao wanaamini hawawezi kumiliki makampuni makubwa kama ilivyo kwa wengine. Hofu yao ya kwamba hawawezi imewafanya wawe hapo walipo leo na wale ambao waliamini kwamba wanaweza, wanazidi kupiga hatua mbele.
Nikiendelea pale nilipoishia wiki iliyopita ni kwamba, kama wewe ni mfanyabiashara, amini kwamba unaweza kuwa mfanyabiashara maarufu na kwa jitihada zako utafika huko. 
Kama wewe ni mwanafunzi, amini unaweza kufika chuo kikuu na kuwa miongoni mwa wasomi wakubwa nchini kama tu utaweka jitihada zako katika masomo.
Nalazimika kusema haya kutokana na ukweli kwamba, kuna watu ambao wana uwezo mkubwa sana wa kufanya mambo lakini wameendelea kuishi  chini ya kiwango kutokana na udhaifu wa imani zao kwamba wao hawawezi. 
Wapo wanafunzi ambao kila siku wanafeli mitihani yao na wanaikubali hali hiyo kwa sababu wameshaweka akilini mwao kwamba kufaulu kwao ni ndoto ya mchana na wapo waliopangiwa kufaulu kila siku.
Kuna wakulima ambao wameridhika kuendesha shughuli zao za kilimo kwa kutumia zana duni huku wakiamini haitatokea siku wao wakatumia matrekta na zana nyinginezo za kisasa. Hizi ni imani potofu ambazo zimekuwa zikiwakwamisha wengi kupiga hatua mbele. 
Nihitimishe kwa kusema kwamba,anza leo kuishi kwa malengo. Weka mikakati ya kutimiza malengo yako, ongeza jitihada katika shughuli zako za kila siku na amini kwamba ipo siku Mungu atakunyooshea mkono na wewe kuwa miongoni mwa watu waliofanikiwa.
Siyo wakati wa kuridhika kuishi maisha yaliyotawaliwa na dhana ya siwezi! Hivi kama utaishi kwa dhana hiyo wakati wengine wanaweza huoni kwamba utakuwa na kasoro? Ni vema basi makala haya yakakuzindua na kuanza kutimiza wajibu wako huku ukiamini kwamba UNAWEZA! Waingereza wanasema, ’play your part it can be done’!


CHANZO: GLOBAL PUBLISHERS

2 comments:

  1. be blessed

    festus kahaya
    author( http://tanzaniagospel.blogspot.com )

    ReplyDelete

Thank you for your comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...