Social Icons

Tuesday, June 26, 2012

NENDA BABA KATUWAKILISHE.....



Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Willibrod Peter Slaa.

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Willibrod Peter Slaa amealikwa kuwa mmoja wa wanajopo (panelists) wanne, kutoka Mabara ya Afrika, Asia, Amerika Kusini na Ulaya, watakaojadili mada isemayo “Demokrasia Shinikizoni (democracy under pressure)” nchini Ujerumani.


Katibu Mkuu Dkt. Slaa ambaye amesafiri jana jioni kuelekea Ujerumani, atakuwa pamoja na wanajopo wenzake wengine ambao ni Prof. Dr. Kyaw Yin Hlaing (Academic Director Myanmar Egress; kutoka Rangum/Myanmar), Dkt. Aliaksandr Milinkiewitsch (Chairman, Movement for Freedom; kutoka Minsk/ Belarus), Gavana Henrique Capriles Radonski (Leader of the Opposition Movement Mesa de la Unidad Democratica; kutoka Carcas/ Venezuela).


Mjadala wa mada hiyo ya Demokrasia Shinikizoni, itakuwa ni sehemu ya sherehe za miaka 50 za Siku ya Shirika la Konrad-Adenauer-Stiftung (KAS Day) katika mahusiano yake ya kimataifa na wadau wake mbalimbali kutoka nchi 80 duniani.
Mwenyekiti wa wanajopo katika kuendesha mjadala huo ni Christoph Lanz (Director of Global Content; Deutsche Welle, Berlin/ Germany)
Sherehe hizo pia zitahudhuriwa na Kansela wa Ujerumani, Dr. Angela Merkel, Rais Mstaafu wa Chile, Seneta Eduardo Frei Ruiz-Tangle na Rais Mstaafu wa Bunge la Ulaya ambaye pia ni Mwenyekiti wa KAS, Dr. Hans-Gert Pottering.


Shirika la KAS linatimiza miaka 50 tangu lilipoanza rasmi kujihusisha na ukuzaji wa demokrasia, uhuru, amani maendeleo na haki. Kwa muda wote huo limekuwa likifanya kazi na wadau katika nchi mbalimbali duniani kutimiza malengo hayo tajwa.
Mpaka sasa KAS ina ofisi 80 sehemu mbalimbali duniani (pamoja na Tanzania), ikishirikiana na wadau wake katika kuendesha miradi inayohusiana na malengo hayo katika nchi 120.


Katika kusherehekea Jubilee ya Miaka 50 ya Siku ya KAS itakayofanyika Juni 27, 2012, shirika hilo limeamua kukutana na wadau na marafiki zake ambao pia wamekuwa wakitoa mchango mkubwa katika utendaji kazi wa KAS katika shughuli za kupigania demokrasia na maendeleo kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa nchi husika.
Katika mada ya “Demokrasia Shinikizoni”, wanajopo watajadili changamoto zinazowakabili watetezi wa demokrasia katika tawala mbalimbali zinazotumia njia dhalimu zinazobana upanukaji wa demokakrasia ambayo ni msingi muhimu wa maendeleo ya watu.


Imetolewa Juni 25, 2012, Dar es Salaam na;
Tumaini Makene
Afisa Habari, CHADEMA  

4 comments:

Thank you for your comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...