Social Icons

Wednesday, January 30, 2013

UKIACHWA NA MPENZI JIULIZE UNA KASORO GANI?


Kusema ukweli nitakuwa mchoyo wa shukrani kama sitachukua nafasi hii kumshukuru Mungu kwa mema ambayo amekuwa akinitendea katika kila siku ya maisha yangu. Hakika Mungu ni mwema na nitaendelea kumtukuza katika siku zote za maisha yangu.
Mpenzi msomaji wangu, hivi ushawahi kukaa chini na kujiuliza kwamba, kama yasingekuwepo mapenzi ulimwenguni binadamu wangeishi vipi? Kimsingi ni swali gumu na hakuna anayeweza kulitolea jibu la moja kwa moja. Ni sawa na wanaume wanavyojiuliza kwamba wasingekuwepo wanawake wangeishije.


Ninachotaka kukizungumzia leo ni kwamba, mapenzi yamekuwa yakiwasumbua walio wengi katika maisha yao hadi wengine kufikia hatua ya kujilaumu kwa nini wameingia katika ulingo huo. 
Wapo waliopoteza maisha kwa sababu ya mapenzi, wapo waliochanganyikiwa na wengine kuathirika tu kisaikolojia kwa sababu ya mapenzi. Pia wapo walioachishwa kazi kwa sababu ya mapenzi. Mimi nasema, mapenzi usipokuwa makini nayo ni kitu hatari sana kwenye maisha yako.
Lakini sasa licha ya mapenzi kuleta matatizo kwa binadamu, bado tunaambiwa utakuwa peke yako kwa muda fulani wa maisha yako lakini mwishowe utatakiwa kutafuta mwenza ambaye utaishi naye kama mume na mke.
Swali la kujiuliza ni kwamba, je kama kila unapoingia katika mapenzi unaumizwa na mtu ambaye umempenda na ungetamani siku moja muoane, kuna ulazima wa kuendelea kung’ang’ania penzi lake? 



Na kama utaendelea kuling’ang’ania penzi la mtu ambaye anakuumiza kila wakati bila kujali, itakuwa inaleta maana? Mimi sijui lakini naamini wewe msomaji unajua zaidi.
Kimsingi katika maisha ya sasa hasa kwa wale ambao bado hawajaolewa au kuoa, wanatakiwa kuwa tayari kuumizwa kwanza kabla ya kumpata yule mwenza mweye mapenzi ya dhati kwao. 
Mapenzi ya sasa yamejaa usanii wa hali ya juu kiasi kwamba ukifanya uchunguzi wa utabaini wengi walio katika uhusiano wa kawaida yaani ‘boyfriend & girlfriend’ wanapitisha wakati lakini uwezekano wa wao kuja kuoana ni mdogo.
Unaweza kuwa katika uhusiano na mtu akawa anakuonesha mapenzi ya kweli mpaka mwenyewe ukajiona mwenye bahati lakini kumbe mwenzako anajifanyisha tu.  
Sasa utajuaje kwamba huyo uliyenaye hana mapenzi ya dhati kwako? Hapo ndipo penye ugumu na ndiyo maana wakati mwingi tunakuwa na imani tu. Tunaamini kwamba, kwa sababu ya hiki ni kile anachonifanyia mpenzi wangu, naamini ananipenda.



Tutambue tu kwamba mapenzi ya kujifanyisha hayawezi kuchukua muda. Utadanganya leo, kesho lakini ipo siku mpenzi wako atabaini tu kwamba amedondoka katika penzi lisilo sahihi na hapo ndipo yaweza kuwa mwisho wa penzi hilo la bandia.
Ninachotaka kukushauri wewe msomaji wangu ni kwamba, inapotokea umeingia katika uhusiano wa kimapenzi na mtu kwa lengo la kutaka kuoana kisha yeye akaja kukuumiza kwa kukufanyia mambo ambayo siyo ya kibinadamu, chukulia kwamba ni safari ya kuelekea kumpata mwingine mwenye mapenzi ya dhati kwako. 
Najua utaumia sana kwani nayaelewa maumivu yake lakini sasa kutakuwa hakuna jinsi kwani kama yeye kaamua kukuacha huna nafasi ya kulirejesha penzi lake hivyo unatakiwa kukubaliana na hali hiyo.



Ila sasa baada ya kuumizwa, hutakiwi kukurupuka kutafuta mtu mwingine kwa lengo la kujaza nafasi hiyo. Hiyo ni mbaya sana kwani unaweza kujikuta tena unaingia katika penzi chungu kuliko hata lililopita. Kaa chini jiulize, mpaka kufikia mpenzi wako kukuacha ni wewe mwenye makosa? 
Kama ni wewe lazima ujute kwanza na kuwa tayari kubadilika. Lakini kama utabaini hukuwa na kosa lolote bali laazizi wako huyo kaamua tu kukuumiza kwa sababu zake mwenyewe anazozijua, hilo muachie Mungu, yeye ndiye atakulipa.




1 comment:

  1. Kweli Joy huwa wengi wanaumia hasa pale wanapoachwa na hatimae pasipo kujiuliza wanachukua hatua ya kujiua badala kujiuliza kwann, lkn pia wapo wanajua chanzo lkn hawataki kukabiliana na matokeo, sijui unawashauri nn hao?

    ReplyDelete

Thank you for your comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...