Social Icons

Monday, February 4, 2013

MAFANIKIO NI LAZIMA LAKINI SI KWA NJIA ZISIZO HALALI!
KAMA wewe ni mmoja wa wafuatiliaji wa karibu wa makala zangu ambazo nimekuwa nikiziandika kupitia safu hii, utakubaliana nami kwamba nimekuwa nikizungumzia suala la mafanikio katika maisha. Msisitizo ukiwa ni katika kufanya kazi kwa bidii na kuwa na malengo thabiti.
Nimekuwa nikiweka mkazo katika kufanya kazi kwa sababu naamini bila kufanya kazi tena kwa bidii, mafanikio hayawezi kuja.
Tunaamini miujiza ipo lakini katika hili usitarajie muujiza wowote unaoweza kutokea na kukufanya wewe ukaukata kimaisha bila kufanya kazi.


Haijalishi unafanya kazi gani kwa sababu nina ushahidi kwa kijana mmoja aliyeanza  kwa kuuza urembo lakini sasa hivi anamiliki maduka mawili na gari moja la mizigo.
 Huyu alichagua mafanikio na aliamini kwamba kufanikiwa kwake kutatokana na kuuza urembo huku malengo yake yakiwa ni kuwa mfanyabiashara mkubwa. Kwa kuwa alikuwa na nia hatimaye amefanikiwa bila kumuibia wala kumdhulumu mtu. Haya ndiyo tunayaita mafanikio ya kweli. 
Lakini sasa linapozungumziwa suala la kutafuta maisha mazuri na yenye mafanikio, wapo watu ambao wanakuwa na dhana potofu ya kwamba, kuukata kimaisha kwa kufanya kazi kihalali ni ndoto huku wakieleza kuwa, walio wengi ambao wana mafanikio makubwa ukifuatilia kwa undani utakuta baadhi yao walidhulumu au walifanya ‘madili’ ambayo huenda yaliwahatarishia maisha yao.


Kwa dhana hii kuna watu huko mtaani sasa wamejenga akilini mwao kwamba, kwa kuuza nyanya mtu hawezi kufanikiwa mpaka ujiingize kwenye uuzaji wa dawa za kulevya na kazi nyingine za namma hiyo.
Hii ni dhana potofu kabisa na ninachoweza kueleza hapa ni kwamba, zipo kazi nyingi tu halali ambazo ukizifanya kwa nguvu zote na kwa malengo unaweza kuwa na mafanikio makubwa kama iliyokuwa kwa kijana ambaye nimemzungumzia mwanzoni mwa makala haya.
Huwa najiuliza bila kupata jibu kwamba, hawa wanaodhani kufanya kazi zisizo halali ndiyo kujipatia mafanikio walishawahi kujiuliza hatima ya maisha yao itakuwaje?
Kwa sababu leo hii wewe ni milionea kwa kazi ya ujambazi katika miji mbalimbali lakini kila jambo lina mwisho, sasa itakuwaje ile siku ambayo utaingia mikononi mwa wananchi wenye hasira kali? Hakutakuwa na kingine zaidi ya kifo. Sasa kama ni hivyo, iweje uhatarishe maisha yako wakati zipo kazi nyingine za kufanya na ukafanikiwa?


Utambue tu kwamba, wanaojipatia pesa kwa kufanya kazi kama vile za kuuza madawa ya kulevya, bangi, utapeli, uchangudoa na shughuli nyingine za namna hiyo maisha yao si ya furaha kama watu wanavyodhani. Wanaishi maisha ya wasiwasi huku wakihofia usalama wa maisha yao.
 Uchunguzi unaonesha kwamba,  wengi wanaofanya biashara hizo haramu mwisho wao huwa mbaya sana ambapo baadhi yao huishia kuuawa, kufa ama kufungwa jela.
Nenda kwenye magereza leo hii utakuta waliojaa huko wanatuhumiwa kwa ujambazi, wizi, uuzaji wa madawa ya kulevya, watu ambao walidhani kwa kufanya hivyo wanaweza kuyafanya maisha yao yakawa mazuri kumbe ndiyo wanajiweka katika wakati mgumu zaidi.
Mimi nadhani zipo kazi nyingi tu ambazo unaweza kuzifanya na kufanikisha ndoto zako bila kuiba kitu cha mtu wala kudhulumu. Ni wewe tu kuamua kutumia akili yako, nguvu zako pamoja na maarifa aliyokujaalia Mungu katika kufanya yale ambayo unaamini kabisa unaweza kufanikiwa na kuishi maisha ya amani yaliyojaa furaha.


 Siyo mpaka uibe ndiyo unaweza kufanikiwa, siyo lazima uuze madawa ya kulevya wala kuuza mwili wako ndiyo ufanikiwe. Fahamu kwamba wapo watu wengi waliopata fhkgjgkmafanikio makubwa kwa kupigana kihalali.
Nihitimishe tu kwa kusema kwamba, kuna kila sababu ya kubadilika na kuangalia njia sahihi ambazo zinaweza kukufanya ukapata mafanikio makubwa katika maisha yetu. Chanzo: Global Publishers

No comments:

Post a Comment

Thank you for your comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...